Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ndugu Gerald Msabila Kusaya leo Mei 5, 2025 amepokea vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 43.5 kutoka Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la AHF ambalo linajihusisha na mkakati wa kufanikisha udhibiti wa HIV na UKIMWI Duniani.
“AHF ni wadau wetu wakubwa katika mapambano dhidi ya HIV na UKIMWI, ninawashukuru kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mara, Mhe Kanali Evans Mtambi, ninatoa ahadi kuwa tutavitunza vifaa hivi vizuri, vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ninaposhukuru hapa maana yake tunaendelea kuomba tena, kama mkipata tena uwezo huo msisite kutoa msaada zaidi.
Ndugu Kusaya amelishukuru Shirika la AHF kwa msaada huo utakaosaidia wataalamu wa afya kutoa huduma bora kwa wananchi katika mapambano dhidi ya HIV/UKIMWI katika maeneo yao.
Bwana Kusaya amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Tarime na Rorya kutunza vifaa hivyo na vifanye kazi iliyokusudiwa ili mabadiliko yaonekane kwa yale malengo ambayo hayajafanikishwa yafanikishwe.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Dkt. Khalifan Lekizenda, ameeleza kuwa vifaa vilivyopokelewa ni kwa ajili ya Vituo vya Afya vya Utegi na Changuge ni muhimu katika kuboresha huduma kwa wanan.
“Msaada huu ni muhimu ili kuboresha huduma kwa wananchi, mathalani wataalamu watatumia pikipiki kuwatafuta wagonjwa waliotoroka dawa ili waendelee na matibabu na kompyuta zitasaidia katika kuhifadhi taarifa za wagonjwa wakati televisheni itasaidia katika kutoa elimu ya afya na namna ya kujikinga” amesema Dkt. Lekizenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Dkt. Amini Wasomana amesema vifaa vilivyopokelewa ni kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Nyangoto kilichopo katika eneo la Nyamongo.
“Ninashukuru kwa kupokea msaada wa vifaa hivi na niahidi kwa niaba ya wenzangu vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa” amesema Dkt. Wasomana.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Kudhibiti UKIMWI na magonjwa ya Ngono na homa ya Inni Mkoa wa Mara Dkt.Omari Gamuya amewashukuru wadau kwa vifaa walivyotoa,
“Hivi ni vifaa muhimu kwa VVU na UKIMWI na bado mpaka sasa kwa utafiti wa mwaka wa 2022/2023 Mkoa wa Mara una maambukizi asilimia 5 ambayo ni juu ya hali ya wastani wa maambukizi ya kitaifa.” Amesema Dkt. Gamuya.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkazi wa AHF Tanzania Bi Aika Mtui amesema kuwa shirika lao linafanya kazi kwa miaka karibu 40 sasa dunia nzima.
“Kwa sasa tupo katika nchi 52, tunashirikiana na Wizara ya Afya ya Tanzania kwa magonjwa ya Kifua Kikuu na magonjwa yote ya ngono kwa mikoa miwili ya Mara na Simiyu baada ya kufanya uchambuzi yakinifu ili kuboresha huduma hizo.” Amesema Bi. Mtui.
Vifaa vilivyopokelewa ni kompyuta za mezani zenye thamani ya shilingi milioni 15,222,000/=, Simu za mkononi za kisasa zenye thamani ya shilingi milioni 2,690,000/=, printa zenye thamani ya shilingi 6,018,000/=, luninga zenye thamani ya shilingi 5,133,000/=, vihifadhia kumbukumbu venye thamani ya shilingi 672,000/=, pikipiki zenye thamani ya shilingi milioni 13,500,000/=.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Zabron Masatu, baadhi ya watumishi kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Halmashauri za Rorya na Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa