Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi leo amempokea ofisini kwake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara na Rais wa Klabu ya Timu ya Mpira wa Kikapu ya Fox Divers Mhe. Esther Matiko akiambatana na viongozi wengine wa klabu hiyo waliokuja kukabidhi kombe la ushindi wa timu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania.
Akizungumza baada ya kupokea kikombe hicho, Mhe. Mtambi amempongeza Mhe. Matiko kwa kazi kubwa anayoifanya kuinua vipaji vya vijana na kushughulikia masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika Mkoa wa Mara.
“Ninakupongeza sana Mhe. Matiko na taasisi ya Matiko Foundation kwa namna mnavyojitoa kushughulikia masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi na kumhakikishia kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara inaunga mkono shughuli zote za kimaendeleo bila kujali itikadi za kisiasa.
Mhe. Mtambi ameipongeza Klabu ya Fox Divers kwa ushindi wao katika Ligi ya Klabu Bingwa ya Mpira wa Kikapu Tanzania na kufuzu kuwania ubingwa wa dunia katika mashindano yatakayofanyika mwaka huu.
Mhe. Mtambi amemuomba Mhe. Matiko kusaidia jitihada za Serikali ya Mkoa za kuwahamasisha wazawa wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo na kuwekeza katika Mkoa wa Mara ili kukuza uchumi wa Mkoa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Fox Divers Bwana Aloyce Renatus amesema Klabu hiyo ilipata ushindi katika fainali zilizofanyika katika uwanja wa Chinangali, Mkoani Dodoma tarehe 14 Desemba, 2024.
Bwana Renatus amesema kutokana na ushindi huo Klabu hiyo imefanikiwa kuchaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika yatakayofanyika katika nchi ya Rwanda kuanzia tarehe 14 Desemba, 2025.
Bwana Renatus amesema kwa sasa timu hiyo inaendelea na maandalizi ya kuwania ubingwa wa Afrika na ikishinda itakuwa imeutangaza Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mhe. Matiko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa mapokezi mazuri na ushirikiano anaoupata kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kumuomba Mhe. Mtambi awe mgeni rasmi tarehe 28 Februari, 2025 katika ufungaji wa mashindano ya Matiko Cup yanayoendelea katika Wilaya ya Tarime.
“Shughuli mbalimbali zitapamba ufungaji huu ikiwemo mashindano ya nyama choma na tunaangalia kama tutaweza kumleta msanii mkubwa aweze kutumbuiza wakati wa shughuli hiyo” amesema Mhe. Matiko.
Hili ni kombe la pili Mhe. Matiko anakabidhi kwa Mkuu wa Mkoa baada ya mwaka 2024 Mhe. Matiko kukabidhi kombe la ushindi la Bunda Queens ambayo yeye alikuwa ni mlezi wake baada ya kushinda katika mashindano kama hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa