Afisa Utamaduni Mkoa wa Mara mwalimu Makondo Makondo amelishukuru Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara Mkoa wa Mara, akisema mafunzo haya yanasaidia kutoa mwanga wa uendeshaji wa shughuli za Utamaduni, Sanaa na Biashara na huku kwa sasa Sekta ya Sanaa imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya taifa, ndani na nje ya Tanzania.
“Unajua fursa za sanaa zipo nyingi, hapa tumeambiwa kuwa Michezo ya Sarakasi umekuwa unafanya vizuri kimataifa hata matamasha makubwa makubwa duniani, wanasarakasi wa Tanzania wamekuwa wanashiriki kila mara matamasha makubwa japokuwa kwa ndani ya taifa letu mchezo huu umekuwa ukitazamwa wa kawaida mno, mchezo huu nao ni fursa kubwa kwa vijana wa Watanzania.”
Mwalimu Makondo aligusia juu ya matumaini yake makubwa baada ya mafunzo haya ya siku mbili, maafisa biashara kutoka Halmashauri za Mkoa wa Mara watakuwa na uwanja mkubwa katika kuelimisha jamii juu ya fursa za sanaa kibiashara, pia kutaisaidia serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka BASATA Ndugu Mrisho Mrisho ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Masoko amesema “fursa za kibiashara katika sanaa zipo nyingi na kama zikitumika vizuri, inaweza kusaidia sana vikundi hivi kujipatia pesa baada ya kusajiliwa huku wakizingatia sheria za nchi na kanuni zote bila ya kuvunja sheria hizo nayo mifumo ya serikali ikisomana.”
Ndugu Mrisho amesema kuwa mafunzo yao yanajikita katika mambo kadhaa ikiwamo kuzijengea uwezo Halmashauri kuhusu vyanzo vya mapato na Leseni za Biashara za kazi za sanaa.
Kwa upande wake Bi Sabaha Hamim kutoka Idara ya Utawala ya BASATA amesema kuwa lengo la Serikali ni kuweza kuwafikia wadau wote huku BASATA na TAMISEMI zikisomana na kukusanya mapato ambayo yatatumika katika kulijenga Taifa.
Kwa upande wake Afisa Utamaduni Kutoka Halmashauri ya Serengeti Jumanne Majori amesema kuwa fursa kadhaa za sanaa zipo katika Halimashauri yake na anatarajia baada ya mafunzo haya fursa hizo atazitumia vizuri.
Kwa upande wake Afisa Biashara Kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara Bibi Rebeka Mdodo amesema kuwa Sekta ya Sanaa ni mojawapo ya biashara ambayo kwa sasa inakuwa kwa kasi huku vijana wengi wameanza kunufaika na kazi zao za Sanaa ikiwemo ngoma za asili, muziki, uchongaji na kadhalika.
“Kwa mwaka wa 2021 Sekta ya Sanaa na Burudani nchini Tanzania ilikuwa kwa asilimia 19 huku ikifuatwa na Sekta ya Nishati ambayo ilikuwa kwa asilimia 10 na kwa mwaka wa 2022 Sekta ya Sanaa na Burudani pia ilikuwa kwa asilimia 19 na nafasi ya pili ilishikwa na Sekta ya Madini na kwa asilimia 10. Kwa hiyo Sanaa na Burudani siyo jambo la kulipuuza kabisa” amesema Bibi Mdodo.
Mkoa wa Mara umekuwa na utajiri mkubwa wa sanaa na utamaduni ambapo eneo hili linavikundi kadhaa vya sanaa tangu ngoma za asili, wasanii wa muziki, sanaa za mikono na sanaa mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa