Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Kanali Evans Alfred Mtambi amesisitiza utoaji wa chakula cha mchana shuleni kwa kila mwanafunzi, huku wananchi wakiambiwa wahakikishe hilo linafanyika, shabaha ni kuongeza ufaulu na kuondoa utoro wa wanafunzi shuleni.
Haya yamesemwa Aprili 30, 2025 katika viwanja vya Mkendo Manispaa ya Musoma ambapo Kanali Mtambi alikuwa akikabidhi madawati kadhaa kwa shule za msingi na sekondari.
“Nawakumbukusha suala la chakula cha mchana mashuleni, angalau mlo mmoja, hili suala halikwepeki, hili ni lazima kwa wana Mara wote, nawaombeni tuhakikishe chakula cha mchana kinachangiwa na kila mzazi/ mlezi mwenye mtoto shuleni kwetu.
Ninaomba nisisikie ubadhilifu wa chakula hicho, ninasema wazi sitomvumilia mtu yoyote atakayefanya ubadhilifu wa chakula cha wanafunzi shuleni.”
Kanali Mtambi alisisitiza Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuhakikisha zinakamilisha kutengeneza madawati yaliyopungua na wanafunzi wa Mkoa wa Mara ni mwiko kukaa chini.
“Tangu jana nilikuwa na vikao na viongozi wezangu juu suala hili hili, nasisitiza kuwa hakuna mtu atakayevumiliwa kwa uzembe huu na ndiyo maana leo nimekuja kukabidhi madawati haya yaliyotengenezwa na wadau mbalimbali” amesema Mhe. Mtambi
Awali akisoma taarifa ya Manispaa ya Musoma Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Mwalimu Bakari Sagini alisema kuwa Manispaa ina shule 65 ambapo shule za msingi ni shule za sekondari ni 21.
Bwana Sagini ameeleza kuwa shule hizo zina wanafunzi 55,764 ambapo wanafunzi wa shule za msingi ni 38,212 na wanafunzi wa shule za sekondari ni 17,552 na Manispaa ya Musoma ina upungufu wa madawati 4,406.
“Tunamshukuru Mbunge wa Musoma Mjini Mhe. Vedasto Mathayo na wadau wengine kwa kufanikisha zoezi hili ambalo litapunguza changamoto ya madawati katika Manispaa ya Musoma” amesema Bwana Sagini.
Hafla ya kukabidhi madawati imehudhuliwa na viongozi kadhaa wa Chama na Serikali, huku wanafunzi wa shule zinazopokea madawati hayo walikuwepo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa