Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara leo tarehe 20 Juni, 2025 wamejengewa uwezo kuhusu Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa, masuala mbalimbali ya kiutumishi, huduma zinazotolewa na Shirika la Bima ya Maisha la SANLAM na Benki ya NMB katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi kuhusiana na masuala ya rushwa na namna ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa katika maeneo ya kazi.
“Lengo la mafunzo haya ni kukumbushana masuala muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kupambana na rushwa katika taasisi yetu na hususan mwaka huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu ameishukuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara pamoja na wadau wengine waliofika kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo muhimu kwa watumishi na kuwataka watumishi kufuatilia kwa ukaribu na kuyazingatia mafunzo hayo katika utendaji wao wa kazi.
Aidha, Dkt. Masatu ameishukuru Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu kwa ajili ya watumishi na kuitaka Idara hiyo kuandaa tena wakati mwingine mafunzo kuhusu magari kwa ajili ya madereva.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Mohamed Shariff amesema wadau mbalimbali wanawajibu wa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa katika taasisi zao na hivyo kuitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kutekeleza majukumu yake kulingana na mwongozo wa mkakati huo.
Bwana Shariff amesema chanzo kikuu cha rushwa ni ukiukwaji wa maadili kwa maslahi binafsi na ili kupunguza tatizo la rushwa sehemu za kazi, Serikali ilitoa mwongozo wa kila taasisi kuwa na Kamati Maalum ya Menejimenti na Kamati ya Uadilifu ili malalamiko ya ndani na nje ya taasisi yaweze kufanyiwa kazi na mianya ya rushwa kuzibwa.
Watumishi pia wamejengewa uwezo kuhusu ujazaji wa taarifa katika mfumo wa PEPMIS, utunzaji wa magari, mabadiliko ya muundo wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa yatakayoanza Julai, 2025, uandaaji wa taarifa baada ya kufanya ufuatiliaji katika Wilaya na Halmashauri.
Aidha, watumishi hao wamepewa pia mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika la Bima ya Maisha la SANLAM na Benki ya NMB na kuhamasishwa kuchangamkia fursa mbalimbali zitolewazo na taasisi hizo.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, Makatibu Tawala wa Wilaya, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na ofisi za Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, maafisa kutoka TAKUKURU, Benki ya NMB na Shirika la Bima la SANLAM.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa