Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 28 Machi, 2025 amefanya ziara Wilaya ya Butiama na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa katika kijiji cha Butiama na kuitaka Halmashauri kutekeleza ujenzi wa majengo hayo usiku na mchana kuanzia leo.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara umepokea maelekezo ya Serikali kuwa shule hiyo itaanza kupokea wanafunzi kuanzia tarehe 22 Aprili, 2025 na hivyo ni lazima ujenzi wake ufanyike usiku na mchana ili majengo yakamilike kabla ya tarehe hiyo.
“Kuanzia leo, ujenzi katika mradi huu uongezwe kasi, ufanyike usiku na mchana ili Mkoa uweze kutekeleza maagizo ya Serikali na uwe tayari kupokea wanafunzi wa shule hii tarehe 22 Aprili, 2025” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutafuta uwezekano wa kufunga umeme wa muda katika mradi huo wakati Mkoa ukiendelea kuifuatilia TANESCO kuhusiana na kuleta umeme katika mradi huo.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mgango Kiabakari kuboresha huduma za maji katika mradi huo na kumtaka Mkurugenzi kuongeza matanki ya kuwekea maji ili yanapokatika ujenzi uweze kuendelea.
Akizungumza baada ya kutolewa maagizo hayo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amesema maagizo ya Mkuu wa Mkoa yamepokelewa na kabla ya TANESCO kupeleka umeme katika eneo hilo, watatumia umeme mbadala kutekeleza ujenzi huo nyakati za usiku.
“Tutaanza ukamilishaji wa majengo muhimu kwa shule hiyo kama vile madarasa, mabweni, matundu ya vyoo huku majengo mengine yaliyopo katika mradi huo yakiendelea kujengwa” amesema Bwana Bulenga.
Bwana Bulenga amesema kwa sasa majengo mengi yanayojengwa yapo katika hatua nzuri na changamoto ya upatikanaji wa vifaa na maji imetatuliwa na kuelezea matumaini yake kuwa majengo mengi yanaweza kukamilishwa hadi tarehe hizo zilizopangwa na Serikali.
Bwana Bulenga amesema kwa tarehe 22 Aprili, 2025 wanategemea kupokea wanafunzi 160 na kati yao wavulana ni 80 na wasichana ni 80 na kuongeza kuwa miundombinu iliyopo ikikamilika itatosha kwa kiasi hicho cha wanafunzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Mhe. Peter Wanzagi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo yake kuhusiana na ukamilishaji wa mradi huo na kuahidi kuwasimamia watendaji kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa maelekezo.
“Uzuri fedha zote za kukamilisha mradi huu tunazo, tutajitahidi kuwasimamia watendaji ili mradi huu utekelezwe kwa haraka kama ilivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa” amesema Mhe. Wanzagi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Kaegele amewataka wakandarasi wanaoshinda zabuni kutekeleza kazi walizoomba kwa mujibu wa mikataba ili kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Kaegele amesema kwa sasa Wilaya imeanza kuwaondoa wakandarasi na mafundi ambao wamepata zabuni lakini hawatekelezi mradi kwa wakati na baadaye itawawia vigumu kupata kazi nyingine katika miradi ya Serikali.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Sekondari ya Butiama Mwalimu Grace Isomba amesema Shule hiyo ilipokea shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Mkoa wa Mara Juni, 2024.
Mwalimu Isomba amezitaja changamoto za utekelezaji wa mradi huo kuwa ni pamoja na mafundi waliopewa kazi kusumbua, wazabuni wa vifaa kutokutekeleza makubaliano kwa mujibu wa mkataba yao.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa