Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi leo tarehe 16 Machi, 2025 amewaonya watu wanaochochea migogoro mbalimbali na kuhatarisha amani na utulivu wa wananchi katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ametoa onyo hilo katika ibada ya kumweka wakfu na kuwekwa kitini Askofu wa Pili wa Dayosisi ya Tarime Rev. John Msuma Nyaitara iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Paulo, Mogabiri, Wilaya ya Tarime na kuongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Mara haitamfumbia macho mtu yoyote atakayechezea amani ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Kuna mgogoro wa muda mrefu katika Kata ya Mwema na Nyabichune katika Wilaya ya Tarime na Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa kwa amani. Serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaouchochea mgogoro huo kwa namna yoyote ile ” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amelipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania na hususan Dayosisi ya Tarime kwa kushughulikia utatuzi wa amani wa migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Tarime na kuliomba kanisa hilo kuendelea kutatua migogoro na hususan katika maeneo yenye changamoto.
Mhe. Mtambi amesema mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na kuwataka waumini na wananchi wote kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati wote wa uchaguzi.
Ametumia fursa hiyo kuwahamasisha waumini wa Kanisa la Anglikana Tanzania na wananchi wote kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba kwa kushiriki uchaguzi Mkuu na kujiandaa kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi katika nafasi mbalimbali za ubunge, udiwani na uwakilishi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Tanga Dkt. Mahimbo Mndolwa amewataka waumini wa Kanisa la Anglikana kushiriki mchakato wa uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Hii ni haki yenu ya kikatiba, ninawaomba waumini wote kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi watakaoiongoza nchi yetu, msifungue milango kumruhusu ibilisi atawale” amesema Askofu Mndolwa.
Askofu Mndolwa amewataka wananchi kutunza mazingira ili kujiepusha na ukame na kuipongeza Wilaya ya Tarime kutunza mazingira na kupanda miti ambayo imelifanya eneo hilo kuwa na hali nzuri ya hewa na kusababisha mvua kunyesha pamoja na kuwa eneo kubwa la nchi yetu lina ukame.
Wakati huo huo, Askofu Mndolwa ametangaza maamuzi mbalimbali yaliyofanyika katika kikao cha Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania kilichofanyika Dodoma tarehe 10 Machi, 2025 ambapo kilimchagua Mkuu wa Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo wa Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania (SJUT) ambao watasimikwa hapo baadaye.
Aidha, Askofu Mndolwa amesema kuwa kikao hicho pia kilimchagua Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Kanon George Otieno Lawi ambaye pia amesimikwa katika Ibada hiyo ili kuendelea na majukumu yake na amempongeza Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Kanisa hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa