Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya kumweka wakfu Askofu wa Pili wa Dayosisi ya Tarime Mchungaji John Msuma Nyaitara, Mhe. Mtambi amelipongeza kanisa hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya hapa nchini.
Mhe. Mtambi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa la Anglikana Tanzania katika sekta mbalimbali na inachukulia kwa uzito mkubwa sana mchango wa Kanisa hilo katika maendeleo ya nchi ya Tanzania.
“Mhe. Rais anawapongeza sana viongozi na waumini wote wa Kanisa la Anglikana Tanzania kwa umoja na mshikamano wenu katika kulijenga kanisa lenu na kwa mchango wenu mkubwa katika maendeleo ya Tanzania” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amelitaka Kanisa la Anglikana Tanzania na waumini wake kuendelea kushirikiana na Serikali na jamii kwa ujumla katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania sio tu katika mambo ya kiroho bali katika maendeleo yao kwa ujumla.
Kanali Mtambi amewataka viongozi wa dini, wazazi na walezi kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii kutokana na athari za utandawazi na kuunga mkono juhudi za kutokomeza vitendo vya unyanyasaji wa wanawake, ukeketaji na kupiga vita mila potofu zinazoirudisha nyuma jamii.
Mhe. Mtambi amelitaka Kanisa la Anglikana Tanzania kuendelea kuiombea nchi ya Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali na wananchi wake ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu na kuihamasisha jamii kuwa na hofu ya Mungu katika maneno na matendo yao.
Mhe. Mtambi amesema ameyapokea maombi yaliyotolewa na Kanisa hilo ikiwemo viongozi wa dini kutambuliwa kwa muchango yao, kupewa nafasi ya uwakilishi bungeni, serikali kuondoa kodi katika taasisi za kidini, Serikali kukamilisha barabara ya Tarime- Serengeti na Serengeti Arusha kwa kiwango cha lami na atayafikisha kwa Mhe. Rais ili yaweze kufanyiwa kazi.
Mhe. Mtambi amewasilisha salamu za Mhe. Rais kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Maimbo Fabian Mndolwa, maaskofu na waumini wa kanisa hilo na kuongeza kuwa Mhe. Rais anawatakia heri na baraka katika kuliongoza Kanisa hilo.
Mhe. Mtambi amempongeza Askofu John Msuma Nyaitara kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Askofu wa Pili wa Dayosisi ya Tarime na kumpongeza Askofu Mstaafu Dkt. Mwita Akiri kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Dayosisi ya Tarime na Tanzania kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Askofu wa Pili wa Jimbo la Tarime John Msuma Nyaitaka amesema viongozi wa dini wanaofanya shughuli zao hapa nchini wanafanya mambo mbalimbali ya kujenga amani, umoja na mshikamano katika nchi ya Tanzania na kumuomba Mhe. Rais kutoa tuzo kwa ajili ya kutambua mchango wa viongozi hao.
Askofu Nyaitira ameiomba Serikali kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kuwa na uwakilishi bungeni ili baadhi ya mambo yanayotatiza katika taasisi hizo yaweze kutatuliwa kabla sheria na maamuzi mbalimbali hayajafanyika.
Aidha, Askofu Nyaitara ameitaka Serikali kupunguza kodi katika shule, vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi mbalimbali za dini kwa kuwa vituo hivi vinatoa huduma kwa bei nafuu kwa wananchi na kwa kuwekewa kodi wananchi wanakosa huduma kwa kushindwa kulipia gharama na kuiomba Serikali kutoa ruzuku kwa taasisi za dini ili kuimarisha huduma inazotoa kwa wananchi.
Askofu Nyaitara ameiomba Serikali kukamilisha kwa kiwango cha lami barabara ya Tarime-Serengeti- Arusha ili kufungua utalii na kuwarahisishia usafiri wananchi wa maeneo hayo na kuharakisha maendeleo ya Tanzania.
Ibada ya kuwekwa wakfu na kuwekwa kitini Askofu John Msuma Nyaitara imehudhuriwa na maaskofu, viongozi wa dini na viongozi wa taasisi za Kanisa hilo kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda na Australia na Uganda na viongozi wa Umoja wa Makanisa ya Kikristu Tanzania (CCT) pia wameshiriki.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mh. Juma Chikoka, baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, waumini na wananchi mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa