Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao utambulisho wa kazi na majukumu ya Mamlaka ya Kudhibiti Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchukua tahadhari na kujilinda dhidi ya tishio la kusambaa kwa maabukizi ya ugonjwa wa murbug hapa nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema japokuwa kwa sasa tishio la ugonjwa huo sio kubwa lakini wananchi wachukue tahadhari kwa kuwa ugonjwa huo hauna kinga wala tiba na unasababisha vifo kwa asilimia zaidi ya 80 ya wagonjwa wanaopata maambuki ya ugonjwa huo.
“Japokuwa kwa sasa ni mtu mmoja amegundulika katika Mkoa wa Kagera, lakini bado kuna uwezekano wa uwepo wa wagonjwa wengine ambao bado hawajagundulika au huyo mgonjwa anaweza kuwa ameshawaambukiza watu wengine kabla yeye hajagundulika” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuwasikiliza na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusiana na namna ya kukabiliana na tishio la ugonjwa huo na hususan kuacha baadhi ya tabia za mazoea zilizozoeleka katika jamii na kuanza tena utaratibu wa kunawa mikono maji tiririka na sabuni kila wakati.
Mhe. Mtambi amewataka wataalamu wa afya, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa Halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na tishio la kuenea kwa ugonjwa huo hapa nchini.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe, Ustawi wa Jamii Bwana Erick Yossam Muhigi amesema amesema Mkoa wa Mara unaendelea na utoaji wa Elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa Murbug na hususan baada ya kugundulika mgonjwa mmoja katika Mkoa wa Kagera.
Bwana Muhigi amezitaja dalili za ugonjwa wa murbug kuwa ni pamoja na muathirika kupata homa kali, kuharisha, kuharisha damu, kutapika, kutapika damu na kutokwa na damu katika sehemu mbalimbali mwilini.
“Ugonjwa huu unaenea kwa njia mbalimbali ikiwemo kugusa jasho, mkojo, damu, kinyesi, matapishi, nguo, matandiko, kugusana na mtu aliyeathrika na ugonjwa huo au wanyama walioathirika na ugonjwa huo” amesema Bwana Muhigi.
Bwana Muhigi amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kunawa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyoathirika na ugonjwa huo na kuepuka kula mizoga ya wanyama waliokufa kutokana na uwezekano wa kula nyama ya mnyama aliyeathrika na ugonjwa huo.
Bwana Muhigi amesema ugonjwa huu unasambaa kwa haraka katika jamii na mtu ambaye ameathirika na ugonjwa huu anaanza kuonyesha dalili za kuwa na ugonjwa wa murbug baada ya siku mbili hadi 21 na muathirika huyo anaweza kuwaambukiza wengine hata kama hana dalili za ugonjwa huo jambo ambalo linaongeza kusambaa kwa maambukizi katika jamii.
Bwana Muhigi amesema Mkoa wa Mara umeimarisha udhibiti wa wagonjwa katika mpaka wa Sirari na vivuko vya wananchi kupita kutoka nchi jirani, udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa Musoma na viwanja vigine vya ndege vilivyoko katika Mkoa wa Mara.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama Mkoa, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, maafisa kutoka taasisi mbalimbali, Halmashauri za Mkoa wa Mara, wadau wa kilimo, mifugo na biashara Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa