Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) na kuwataka wakurugenzi kuwasilisha taarifa ya hali ya shule kongwe na mkakati wa ukarabati wa shule hizo.
“Ninataka kujua shule zote kongwe zilizopo katika Halmashauri na hali yake na mikakati ya Halmashauri katika kuzikarabati shule hizo ili kwa ajili ya usalama wa wanafunzi….fedha zipo tuongeze jitihada katika makusanyo” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuwahamasisha wananchi kupeleka watoto shule zitakapofungua Januari, 2025 ili kuwawezesha watoto hao kupata elimu itakayowasaidia kuboresha maisha yao.
“Serikali imewekeza sana na hususan kujenga shule nyingi na kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za awali na kwa sasa Mkoa hauna mapungufu tena ya vyumba vya madarasa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufuatilia fedha za miradi ya maendeleo zilizopokelewa kwenye mamlaka zao ambazo hazijatumika kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa na Serikali na kupanga mikakati ya kutekeleza miradi hiyo.
Mhe. Mtambi pia amewata Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wa Serikali kuboresha mfumo wa upokeaji malalamiko ya wananchi pamoja na kuwatembelea wananchi katika maeneo yao.
Akitoa taarifa kwenye kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amesema idadi ya vyumba vya madarasa vilivyopo vinatosheleza mahitaji ya madarasa kwa mwaka wa masomo 2025 na kuwahamasisha wazazi kupeleka watoto shule.
Bwana Bulenga amesema Mkoa umeweka makadirio ya kuandikisha watoto 82,679 wa elimu ya awali na mpaka tarehe 22 Novemba, 2024 jumla ya watoto 14,329 ambao ni sawa na asilimia 17.33 ya watoto wote wanaotarajiwa kuandikishwa.
Bwana Bulenga amesema Mkoa umekadiria kuandikisha wanafunzi 74,223 wa darasa la kwanza na hadi kufikia tarehe 22 Novemba, 2024 Mkoa umeandikisha wanafunzi 19,022 ambao ni sawa na asilimia 25.62 ya lengo la Mkoa.
Bwana Bulenga amesema Mkoa una jumla ya shule za msingi 979 ma Sekondari 316 na una jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 635,842 na wanafunzi wa Sekondari 134,560.
Bwana Bulenga amesema katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2024 jumla ya wanafunzi 60,261 walifanya mtihani huo na kati yao wanafunzi 47,034 walifaulu na wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2025 wakati wanafunzi 13,227 walifeli.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa