Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepokea tuzo za ubora wa huduma zilizotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI kwa vituo viwili vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Musoma na kuipongeza Manispaa ya Musoma kwa usimamizi wa sekta ya afya.
Mhe. Mtambi ametoa pongezi hizo baada ya Kituo cha Afya Nyasho kushinda tuzo ya utoaji wa huduma kitaifa huku Zahanati ya Kwangwa ikiwa kati ya zahanati 17 bora kitaifa kufuatia tathmini iliyofanywa na wataalamu wa afya hapa nchini.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara ninakipongeza Kituo cha Afya Nyasho na Zahanati ya Kwangwa kwa utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi na kwa ushindi walioupata kitaifa ambao umetuletea heshima katika Mkoa wetu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema inafurahisha kuona Mkoa wa Mara ukitajwa katika mambo mazuri yanayoonyesha uhodari na utendaji kazi wa watumishi wa Mkoa wa Mara katika kuwatumikia wananchi.
Mhe. Mtambi pia ametoa shilingi milioni moja kwa kila kituo kama motisha na kuiagiza Wilaya na Manispaa ya Musoma pia kutoa fedha kwa ajili ya kuwapa motisha watumishi waliofanikisha upatikanaji wa tuzo katika vituo hivyo.
Mhe. Mtambi amezishukuru Wizara za Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kuandaa tuzo hizo ambazo amesema zinatabua juhudi kubwa zinazofanywa na wataalamu katika maeneo mbalimbali kuokoa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amewapongeza watumishi na uongozi wa vituo hivyo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuahidi kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa kutoa shilingi 1,500,000 kwa kila kituo ili kuunga mkono maono ya Mkuu wa Mkoa ya kuwapongeza watumishi hao.
“Hizi ni tuzo ni tuzo za utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kama Wilaya tunashukuru sana vituo vyetu viwili kupata ushindi huu kimkoa na Kitaifa jambo linaloonyesha huduma zetu ni nzuri” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka amesema Kituo cha Afya Nyasho kimekuwa mshindi wa kwanza kati ya vituo vya afya zaidi ya 3,700 vinavyotoa huduma za afya hapa nchini huku Zahanati ya Kwangwa ikiwa miungoni mwa zahanati 17 nchini zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu amesema vituo vya kutolea huduma vilifanyiwa tathmini nchi nzima na matokeo yake Kituo cha Afya Nyasho kimekuwa mshindi wa kwanza kitaifa kati ya vituo vyote vya afya vilivyopo huku Zahanati ya Kwangwa ikiwa miungoni mwa zahanati 17 kitaifa zilizofanya vizuri.
Dkt. Masatu amesema vigezo vya tuzo hizo vilikuwa ni pamoja na usafi wa vituo, ubora wa huduma, upatikanaji wa dawa, utunzaji wa takwimu na taarifa za afya, upatikanaji wa huduma kwa wakati na kadhalika.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyasho Dkt. Richard Majahasi amesema siri ya ushindi huo ni ushirikiano na kujituma kwa wafanyakazi wa kituo hicho katika kuwahudumia wananchi.
“Vigezo vingi vimetumika kuwapata washindi ila ninaamini ushirikiano wa wafanyakazi na kutoa huduma nzuri kwa wateja ndio siri kubwa ya ushindi tulioupata na tunaahidi kuendelea kuboresha huduma ili tukidhi viwango vinavyotakiwa” amesema Dkt. Majahasi.
Dkt. Majahasi amesema kituo chake kina idadi kubwa ya wateja wanaopata huduma hapo lakini wameweza kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji yao na amewashukuru watumishi wa kituo hicho kwa kazi na ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwake.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kwangwa Dkt. Christopher Bilia ameishukuru Serikali kwa kuanzisha tuzo hizo na kuongeza kuwa tuzo hiyo itakuwa chachu ya kuongeza morali ya wafanyakazi wa zahanati hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Bilia amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutoa motisha kwa watumishi waliofanyanikisha upatikanaji wa tuzo hiyo na kuahidi fedha itakayopatikana itatumika vizuri kutoa motisha kwa watumishi wote waliofanikisha upatikanaji wa tuzo hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa