Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amefanya ziara katika Wilaya ya Rorya na kutembelea Shule ya Msingi Radienya iliyoko katika Kata ya Kirogo na kuahidi maboresho makubwa katika miundombinu na idadi ya walimu wa shule hiyo.
“Shule hii tutaifanyia maboresho makubwa hivi karibuni na hususan miundombinu ili mazingira yawe rafiki kwa walimu na wanafunzi na kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha katika shule hii” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amemuagiza Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufuatilia kwa ukaribu maboresho yanayohitajika katika shule hiyo ili kuwashirikisha wadau wa elimu na kuzitumia vizuri fursa zinazotolewa na Serikali katika uboreshaji wa miundombinu ya shule.
Aidha, Bwana Kusaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Bwana Abdul Mtaka kutembelea shule hiyo na kuwasilisha mahitaji halisi ya shule hiyo ofisini kwake na hatua ambazo Halmashauri hiyo itazichukua kwa haraka ili shule hiyo iendelee kutumika wakati fedha za ujenzi wa shule mpya zinatafutwa.
Aidha, RAS amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mara kuitembelea shule hiyo na kujenga barabara na daraja kuweza kupitisha magari na wanafunzi kuingia na kutoka katika shule hiyo.
Bwana Kusaya amewapongeza walimu wanaofundisha katika shule hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwaahidi kuwaboreshea mazingira ya kufundishia na kujifunzia na nyumba za kuishi haraka iwezekanavyo.
Akiwa katika shule hiyo, Bwana kusaya amezungumza na walimu na wanafunzi, amekagua madarasa, vyoo, ofisi za walimu na nyumba za walimu na kujionea uchakavu wa miundombinu ya shule hiyo ya zamani.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Makwasa Bulenga amesema tayari Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imewahamishia walimu wawili wengine katika shule hiyo na barua za uhamisho zipo tayari na wanatarajiwa kuwasili shuleni hapo baada ya muda mfupi.
Bwana Bulenga amewataka walimu kujaza taarifa sahihi za hali halisi ya shule zao kwenye mfumo wa taarifa za shule hapa nchini ili kuweza kupunguza tatizo la uchakavu wa miundombinu ya shule.
“Ukiingia kwenye mfumo, shule hii inaonyesha mambo yake yapo safi, ina vyoo, madarasa ya kutosha na nyumba za walimu, lakini ukija hapa kuona hali halisi kuna darasa moja tu ndio zima majengo mengine yote ni mabovu” amesema Bwana Bulenga.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Rwehumbiza Tresphory Tryphone amesema Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 609 wa madarasa ya awali hadi darasa la saba na walimu watano ambapo mmoja kati yao yupo masomoni na kubakiwa na walimu wanne.
Bwana Tryphone amesema shule hiyo ina vyumba saba vya madarasa ambavyo vyote ni vibovu isipokuwa chumba kimoja kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi na kukamilishwa na Serikali ndio kina hali nzuri na shule ina matundu manne tu ya vyoo ambayo yapo katika hali mbaya.
Aidha, Mwalimu Tryphone amesema Shule hiyo inazo nyumba sita za walimu lakini mbili ni mbovu sana haziwezi kukalika na nyumba nyingine nne ni chakavu lakini bado zinaendelea kutumiwa na walimu wa shule hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Radienya Bwana Stephen Nyakitita amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kuitembelea shule hiyo na kuahidi kuwa viongozi wa Kijiji hicho wataendelea kuwahamasisha wananchi kusaidia katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Bwana Nyakitita ameyataja matatizo makubwa ya shule hiyo kuwa ni barabara ya kuingia shuleni hapo kutokana na uwepo wa korongo kubwa sana ambalo linahatarisha maisha ya wanafunzi wanaotokea upande mmoja wa kijiji hicho wakati wa mvua.
Aidha, Bwana Nyakitita amesema wakati wa mvua magari hayawezi kuingia katika Shule hiyo kutokana na njia zote za kuingia katika shule hiyo kuwa mbaya na kulazimisha vifaa kubebwa kichwani kwa zaidi ya kilomita moja ili kuweza kuingia shuleni hayo.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata wa Kata ya Kirogo Bwana Justine Masau amesema miundombinu ya shule nyingi za kata hiyo ni mibovu sana na ina walimu wachache jambo ambalo liliifanya Kata hiyo kuwa ya mwisho katika mitihani yote ya shule za msingi.
Bwana Masau amesema hata hivyo alikutana na walimu wa shule za Kata hiyo na kupanga nao na mwaka 2023 kata hiyo ilitoka nafasi ya 26 hadi nafasi ya 10 na mwaka 2024 imeshika nafasi ya 12 katika matokeo ya Darasana la Saba.
Bwana Masau amemuomba Katibu Tawala kuwaongeza walimu na kuboresha miundombinu ya shule hizo ili kutoa mazingira bora ya kujifunza na kufundishia.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara aliambatana na baadhi ya Maafisa kutoka ofisini kwake na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa