Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyaburundu na ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kukamilisha mradi huo.
Akizungumza baada ya kukagua na kupokea taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Bwana Kusaya ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha shule hiyo inakamilika ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo.
“Mimi nitakuja tena hapa tarehe 21 Februari, 2024 kukagua utekelezaji wa maagizo yangu ya leo na kama kuna tatizo lolote litakalokwamisha ukamilishaji wa ujenzi wa shule hii nipatiwe taarifa mapema kabla ya muda huo” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amemuelekeza Mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kufuata taratibu za usajiri itakapokamilika ili shule hiyo ianze kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanzia Januari, 2026.
Aidha, Bwana Kusaya amewapongeza wasimamizi wote wa mradi huo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika usimamizi wa ujenzi huo na kuwataka mafundi kuongeza kasi ya ujenzi kwa kuzingatia ubora katika ujenzi wa mradi.
Taarifa ya mradi huo inaonyesha kuwa fedha shilingi milioni 584 zilipokelewa Juni 23, 2024 kutoka katika Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na taratibu za manunuzi zikaanza Septemba, 2024 baada ya kupata kibali cha upanuzi wa vifungu vya Halmashauri hiyo na ujenzi umeanza tarehe 24 Novemba, 2024.
Aidha, taarifa ya mradi huo inaonyesha kuwa majengo 13 yanajengwa na jengo la utawala limeanza kuwekwa tofali baada ya lenta, majengo mengine mawili yameshafungwa lenta, majengo mawili yanatarajiwa kuanza kufungwa lenta na majengo manne yapo kwenye hatua za msingi.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa ujenzi wa mashimo ya vyoo bado haujaanza na mafundi wa kujenga vyoo hivyo wameshapatikana na shughuli ya ufyatuaji wa tofali kwa ajili ya majengo yanayoendelea kujengwa unaendelea katika mradi huo.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa mpaka wakati huo mradi umefikia asilimia 45 ya ujenzi na jumla ya shilingi 142,680,426.76 zimeshatumika kwa ajili ya kulipia vifaa na fedha za mafundi katika mradi huo.
Akizungumza katika mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana George Mbilinyi amesema mradi huo umechelewa kuanza kutokana na kusubiria upatikanaji wa vifungu na wazabuni kutokuomba kazi za mradi huo baada ya kutokana uhalisia wa eneo la mradi huo.
“Mradi huu upo mbali sana na sehemu za kupata mchanga, mawe na kokoto na wazabuni wengi waliokuwa wanaomba wanaomba kwa gharama kubwa kuliko bajeti iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya vifaa hivyo” amesema Bwana Mbilinyi.
Bwana Mbilinyi amesema kwa sasa Halmashauri imefanikiwa kuwapata wazabuni waliokamilisha utekelezaji wa miradi maeneo mengine ambao wamekubali kufanya kazi katika mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyaburundu Bwana Hamis Said Madoro ameeleza kuwa katika eneo hilo mchanga, mawe na kokoto vinapatikana mbali sana na wenyeji wakiwa wanajenga wanaletewa mchanga kwa shilingi 120,000- 130,000 kwa tripu moja.
“Kwa hii bei ya Serikali ya shilingi 75,000 kwa tripu moja wazabuni wote walikataa kwa sababu huku ni mbali sana na wanaona kwa biashara zao haiwalipi” amesema Bwana Madoro.
Bwana Madoro ameipongeza Serikali kwa kujenga Shule hiyo ambayo amesema itawapunguzia wanafunzi umbali waliokuwa wanatembea kufuata shule ya Sekondari iliyopo katika Kata hiyo.
Ziara ya Katibu Tawala katika shule hiyo inafuatia Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi wa Kijiji cha Nyaburundu kuhusu ujenzi wa shule hiyo kuchelewa na kumwelekeza Bwana Kusaya kufuatilia ujenzi wa shule hiyo.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala ameambatana na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na baadhi ya maafisa wa Halmashauri hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa