Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo ametoa shilingi milioni mia moja (100,000,000) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mvua na upepo mkali uliotokea katika Kata 10 za Manispaa ya Musoma tarehe 23 Machi, 2025.
Msaada huo umekabidhiwa leo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi na Mshauri wa Kisiasa wa Mhe. Rais Mhe. Haji Omar Kheir (Mb.) aliyewasili Musoma leo tarehe 26 Machi, 2025 kufuatia maafa hayo.
Akizungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali amesema Mhe. Rais anawashukuru sana wananchi wa Musoma kwa ustahimilivu wao kufuatia maafa hayo na kuwataka kuendelea kuwa na utulivu wakati Serikali ikiendelea kutatua changamoto hiyo iliyojitokeza.
Mhe. Kheir amesema baada ya kupokea taarifa za maafa hayo, Mhe. Rais alitoa maelekezo mahususi ya namna ya kushughulikia maafa hayo na amewatuma washauri wake wa kisiasa kuja kufanya tathmini na kumjulisha hali halisi ya maafa hayo.
Wakati huo huo, Washauri wa Kisiasa wa Mhe. Rais leo wakiwa wanazungumza na waathirika katika kambi maalum ya waathirika hao wamechangia shilingi 3,500,000.00 kwa ajili ya kuwasaidia wathirika wa tukio hilo.
Fedha hizo zimetolewa na Mhe. Mhe. Kheir shilingi 2,000,000.00, Mhe. Alhaj Abdalla Bulembo shilingi 1,000,000.00 na Mhe. Balozi Rajab Omar Luhwavi shilingi 500,000.00
Aidha, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mhe. Vedastus Mathayo ametoa mitungi mikubwa miwili ya gesi na majiko yake kwa ajili ya kupikia katika kambi hiyo na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Ghati Chomete amechangia mchele kilo 100.
Akizungumza katika makabidhiano ya pesa hizo, Mhe. Mtambi amesema wananchi wa Mkoa wa Mara wamefarijika sana kwa moyo wa ukarimu na upendo kwa wananchi aliouonyesha tangu maafa yalipotokea katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ameahidi kuwa fedha hizo na nyingine zitakazotolewa zitatumika vizuri katika kutoa huduma kwa waathirika na kurejesha maisha ya wananchi katika hali ya awali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa amemshukuru Mhe. Rais kwa msaada wa haraka alioutoa kwa waathirika wa maafa hayo na kuongeza kuwa wananchi wa Mkoa wa Mara wanafarijika sana na msaada huo.
Mhe. Chandi amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kutoa msaada kwa wananchi walioathirika na tukio hilo ili waweze kurejea katika hali zao za awali mapema iwezekanavyo.
Mhe. Chandi ameipongeza Serikali ya Mkoa kwa kuwasaidia wananchi kwa haraka na kuwatafutia makazi ya muda wakati jitihada za kuwarejesha katika maeneo yao ya awali zikiendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa