Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki mazishi ya watu nane waliofariki katika mafuriko Mjini Tarime na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika kutoa malalamiko kuhusiana na uchaguzi uliofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Mhe. Mtambi amesema vyama vya siasa vyote 19 vilivyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 vilishiriki kutunga kanuni za uchaguzi ambazo ndio zinaongoza shughuli zote za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sasa.
“Mchakato wa uchaguzi bado unaendelea, kanuni za uchaguzi zimeainisha nini cha kufanya katika kila hatua ya uchaguzi, kwa mujibu wa kanuni hizo kama kuna chama kina malalamiko yanapaswa kuwasilishwa rasmi kwa wasimamizi wa uchaguzi ndani ya siku 30 na yatasikilizwa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amevihakikishia vyama vya siasa kuwa Mkoa wa Mara katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaongozwa na kanuni za uchaguzi kwenye kushughulikia masuala yote ya uchaguzi na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kama wanamalalamiko kufuata taratibu zilizowekwa katika kanuni za uchaguzi.
Aidha, amevipongeza vyama vya siasa, wanasiasa na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ukomavu wa kisiasa waliouonyesha wakati wote wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka kuendeleza amani na utulivu uliopo.
“Katika uchaguzi huu, hamna aliyeshindwa wala aliyeshinda ila wanamara kwa umoja wetu ndio tumeshinda, uchaguzi umepita sasa tuendelee kuishi kama ndugu na kushikamana kama Watanzania bila kujali tofauti za itikadi zetu” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amesema viongozi wateule waliochaguliwa bado hawajaapishwa ili kuendelea na majukumu yao na wataapishwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza ili waweze kuanza kutekeleza majukumu yao katika jamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki amewashukuru wananchi Wilaya ya Tarime kwa ushiriki wao katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na usalama.
Mhe. Kembaki amewashukuru sana wananchi kwa namna walivyotoa ushirikiano katika kipindi chote cha uchaguzi ikiwa ni pamoja na kushiriki kampeni za uchaguzi na baadhi yao kugombea nafasi mbalimbali zilizokuwa zinagombaniwa.
Mhe. Kembaki ametoa pole kwa wafiwa na wote walioathirika na mafuriko hayo na kuipongeza Serikali na Vyombo vya Usalama kwa namna walivyoshiriki katika maafa hayo tangu mafuriko yalipotokea.
Mafuriko makubwa yalitokea kandokando ya Mto Mori katika Kata ya Nyamisangula, Mji wa Tarime na kusomba nyumba nne na watu tisa kupoteza maisha huku watu wawili wakinusurika kifo na madaraja mawili yakiathirika katika eneo hilo tarehe 24 Novemba, 2024.
Mazishi hayo yamehudhuriwa pia na Kamati ya Usalama Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama Wilaya ya Tarime, viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi, Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa