Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha tathmini ya mbio za mwenge mwaka 2024 na kukabidhi tuzo ya pongezi kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa na kinyago kwa Manispaa ya Musoma kwa kushika nafasi ya mwisho kimkoa katika mbio hizo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi kinyago hicho, Mhe. Mtambi ameagiza kinyago hicho kipokelewe na Mkuu wa Wilaya ya Musoma akiambatana na Katibu Tawala, Mkurugenzi wa Manispaa na Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Manispaa ya Musoma.
“Kinyago hiki kikae ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mpaka atakapopatikana Mkuu wa Wilaya mwingine ambaye Wilaya yake itakuwa imefanya vibaya wa kumpokea” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kinyago kilichotengenezwa sio kibaya sana kama alivyoagiza na kuitaka Manispaa ya Musoma kulipa gharama za kutengeneza kinyago hicho ili kutoa fundisho kwa Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara kufanya vizuri zaidi katika mbio za mwenge kwa miaka inayokuja.
Aidha, Mhe. Mtambi ametoa tuzo ya pongezi kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ambayo imeongoza kimkoa kwa kupata alama 73.12 na kushika nafasi ya 59 kitaifa pamoja na kuwa mradi mmoja ulikataliwa katika mbio hizo lakini vigezo vingine ilifanya vizuri.
Mhe. Mtambi amezitaka Wilaya kuwa makini katika maandalizi ya mbio za mwenge za mwaka 2025 na kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mbio za mwenge za mwaka 2024 na kuzipongeza Wilaya ambazo tayari zimeanza kufanya maandalizi.
Akiwasilisha tathmini ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024, Mratibu wa Mbio za Mwenge Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye amesema katika mbio hizo Mkoa ulishika nafasi ya 16 kati ya mikoa 31 iliyopo hapa nchini.
Bwana Baragaye amesema Halmashauri iliyofanya vizuri ni Halmashauri ya Mji wa Bunda iliyopata alama 73.12 na kitaifa ikawa nafasi ya 59 na Halmashauri iliyofanya vibaya ilikuwa ni Manispaa ya Musoma ambayo ilipata asilimia 62.17 na kushika nafasi ya tisa kimkoa na kitaifa ilishika nafasi ya 158.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa changamoto zilizokuwepo ni pamoja na kukosekana kwa nyaraka kwenye baadhi ya miradi, nyaraka zenye mapungufu, uwepo wa stakabadhi zenye mashaka, kuwepo kwa taratibu za manunuzi zilizokiukwa na kutokuzingatia kwa ukamilifu kigezo cha uwezeshaji wa vijana iliyokuwa na vipengele vya mradi wa vijana uliotakiwa kutembelewa na Mwenge na maandalizi ya kongamano la vijana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka ameupongeza Mkoa wa Mara kwa kuanzisha utaratibu huo wa kutoa vinyago kwa wanaofanya vibaya ili kutoa hamasa kwa Wilaya kufanya vizuri zaidi.
Mhe. Chikoka amesema Wilaya ya Musoma imejipanga kuhakikisha kuwa katika miaka inayofuata haitafanya vibaya tena na kuwataka Wakuu wa Wilaya wengine wajiandae kuchukua kinyago hicho.
Kikao cha tathmini ya mbio za mwenge mwaka 2024 na maandalizi ya mbio za mwenge 2025 kimehudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa Mbio za Mwenge wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa