Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA) Bi. Esther Gilyoma amezitambulisha mita mpya ya maji ambazo zitaanza kufungwa katika Mji wa Bunda hivi karibuni zitakazomwezesha mteja kulipia huduma za maji kabla ya kutumia zitasaidia katika kupunguza malalamiko ya kulipia bili za maji.
“Mamlaka imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu bili za maji na sasa tumepata mwarubaini utakaomaliza kero hii kwa kuwawezesha wananchi kulipia maji kabla ya kuyatumia kulingana na uwezo wao” amesema Bibi Gilyoma.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya mita hizo, Bi. Gilyoma amesema mita hizo zitatumika katika maeneo yote yenye mtandao wa maji wa mamlaka hiyo baada ya wananchi kuchangia gharama za kufungiwa mita hizo.
Bi. Gilyoma amezitaja faida za mita hizo kuwa ni pamoja na kupunguza malalamiko ya wateja kulimbikiziwa bili, kumwezesha mteja kupanga matumizi yake ya maji kulingana na kipato chake, kumwondolea mwenye nyumba kero ya kulipa bili ya maji iliyotumiwa na wapangaji baada ya wao kuondoka.
Bi. Gilyoma amewahamasisha wananchi na hususan wenye nyumba zenye wapangaji, taasisi na maeneo ya biashara kuchangamkia kuzinunua mita hizo ili kuwawezesha kupunguza migogoro isiyo ya lazima na BUWSSA na wapangaji wao kutokana na bili za maji.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kwa sasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Bunda na maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hiyo upo kwa asilimia 85 na kwa sasa Mamlaka hiyo inao wateja zaidi ya 10,000.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wazo PIC Technology Limited Bwana Yoweri Maximilian Chacha amesema Kampuni hiyo ni msambazaji wa mita hizo kwa miaka mitatu sasa na imezisambaza katika Mamlaka mbalimbali za maji katika Mikoa ya Mara, Mtwara na Simiyu.
“Mita hizi zina ubora wa hali ya juu na zimepata ithibaki kitaifa na kimataifa na tangu tumeanza kuzifungwa kwa miaka mitatu hatujapata malalamiko kutoka kwa wateja na mamlaka za maji kuhusiana na ubora” amesema Bwana Chacha.
Bwana Chacha amesema mtumiaji wa mita hiyo ataitumia kama ilivyo mita za umeme wa luku kwa kununua token na kuchaji ili kupata huduma za maji kulingana na malipo yaliyofanyika.
Hafla ya mapokezi ya mita hizo zaidi ya 1,000 zitakazofungwa katika Mji wa Bunda imehudhuriwa na watumishi wa BUWSSA na kampuni ya Wazo PIC Technology Limited inayohusika na usambazaji wa mita hizo hapa nchini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa