Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mkoa wa Mara Bwana Makwasa Bulenga leo amefungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea wasimamizi wa shule na walimu wa masomo ya Hesabu na Kiingereza kwa Shule za Msingi na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuleta mabadiliko katika ufundishaji, uelewa na ufaulu wa wanafunzi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Mradi wa Shule Bora yanayofanyika katika Hotel ya Gold Crest, Mwanza, Bwana Bulenga amesema Mkoa wa Mara umejipanga kuboresha uelewa na ufaulu wa wanafunzi katika matokeo ya mitihani mbalimbali ya Shule za Msingi.
“Tuitumie vizuri fursa ya mafunzo haya ili tuweze kuboresha usimamizi na ufundishaji katika shule zetu, bado hatufanyi vizuri sana kama Mkoa na malengo yetu tuwe Mkoa kinara katika ufundishaji na ufaulu katika elimu ya msingi hapa nchini” amesema Bwana Bulenga.
Bwana Bulenga amewataka washiriki kushiriki kikamilifu mafunzo hayo na kwenda kuboresha ufundishaji wa masomo hayo katika maeneo yao ya kazi na kuwaambukiza maarifa hayo walimu wengine waliopo kwenye maeneo yao ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.
Bwana Bulenga amesema kuwa mara nyingi shule zinazofanya vibaya zinalaumu wanafunzi, wazazi, walezi na jamii kutokutoa ushirikiano kwa shule hizo jambo ambalo amesema sio sahihi na kuwataka walimu kutimiza wajibu wao katika ufundishaji, kuwalea wanafunzi na kuihudumia jamii inayowazunguka.
Bwana Bulenga amewataka walimu na wasimamizi wa Elimu Mkoa wa Mara kuitumia vizuri fursa ya kuwa na Mradi wa Shule Bora ambao umekuwa ukifadhili mafunzo mbalimbali kwa walimu na wasimamizi wa elimu katika Mkoa wa Mara kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika maeneo hayo.
“Huu ni mwaka wa tatu, tumekuwa tukipewa mafunzo mbalimbali na Mradi wa Shule Bora na wadau wengine, wakati umefika sasa matokeo ya uwekezaji huu unaofanywa yaonekane kwa wanafunzi wetu” amesema Bwana Bulenga.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Mara Bwana Sam Mwita amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha masomo ya Kiswahili na Kiingereza ili kuboresha uelewa wa wanafunzi na hatimaye ufaulu wao katika mitihani mbalimbali ya ndani na ya Kitaifa.
“Kwa sasa Mkoa haufanyi vizuri sana wala vibaya sana, upo katikati na mafunzo haya yanalengo la kuboresha hali hiyo ili Mkoa uweze kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya mitihani mbalimbali” amesema Bwana Mwita.
Bwana Mwita amesema masomo ya Kiswahili na Kiingereza yanachangamoto nyingi katika uelewa na ufaulu wa wanafunzi na lengo la mafunzo haya ni kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo ili Mkoa wa Mara uweze kufanya vizuri katika ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya shule za msingi.
Kwa upande wake, Mwalimu Eunice Makene, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama amemshukuru Afisa Elimu Mkoa wa Mara kwa kufungua mafunzo hayo na ameushukuru Mradi wa Shule Bora kwa kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kuwa yote watakayojifunza watayafanyia kazi.
“Sisi tunashukuru sana kwa fursa hii ya mafunzo na tunaahidi kujifunza kikamilifu na kwenda kuyafanyia kazi mambo yote tutakayojifunza katika mafunzo haya” amesema Mwalimu Makene.
Mwalimu Makene amewataka walimu walioshiriki mafunzo hayo wanaporudi katika vituo vyao vya kazi kwenda kuboresha ufundishaji wao na kuwaambukiza walimu wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.
Mfunzo hayo yanaongozwa na wataalamu ambao ni Dkt. Martanus Ocholo Omoro Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Dkt. Mjege Kinyota Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na baadhi ya Maafisa wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Maafisa Elimu ya Msingi, Maafisa Elimu Taaluma na Wadhibiti Ubora wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara, baadhi ya Waratibu wa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na walimu wa masomo ya Hesabu na Kiingereza kutoka katika baadhi ya shule za Msingi za Mkoa wa Mara.
Mradi wa Shule Bora unafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia taasisi zake mbalimbali na unatekelezwa katika Mikoa tisa hapa nchini ambayo ni Mkoa wa Mara, Tanga, Simiyu, Pwani, Kigoma, Singida, Dodoma, Katavi na Rukwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa