Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi akiwa ameongozana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara leo tarehe 25 Machi, 2025 ametembelea eneo lililokumbwa na maafa katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na kujionea uharibifu uliotokea kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali tarehe 23 Machi, 2025 usiku.
“ Nimekuja hapa nikiwa nimeongozana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Katibu wa chama cha mapinduzi, viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka mkoani, Manispaa ya Musoma kuwapa pole, kuangalia hali halisi ilivyo na kutoa msaada wa haraka unaohitajika” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewapongeza wananchi wa Manispaa ya Musoma kwa kuwasaidia walioathirika katika maafa hayo, kuwahi kutoa taarifa kwa vyomba vya Usalama na viongozi mbalimbali na kuzipongeza taasisi zote zilizosaidia katika kufanya uokoaji wa haraka katika maeneo mbalimbali.
Akiwa katika eneo hilo, Mhe. Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kukarabati mara moja nyumba ya Bibi Eveline Masuba mkazi wa mtaa wa Makongoro uliopo katika kata ya kitaji ambaye paa la nyumba yake pia limeezuliwa na upepo huo.
Aidha, ameiagiza Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma kuongeza ulinzi katika maeneo yote yaliyoathirika na maafa hayo ili wananchi na mali zao waweze kuwa salama.
Mhe. Mtambi amewatahadharisha wezi na watu wote waliojipanga kuiba katika kipindi hiki cha maafa kwa kuwajulisha kuwa Kamati ya Usalama Mkoa na Wilaya zimejipanga kuimarisha ulinzi na yeyote anayepanga kuiba au kuharibu mali za wananchi na taasisi za umma atakamatwa.
Mhe. Mtambi amewahakikishia wananchi kuwa timu mbalimbali za wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma zitapita katika maeneo yao ili kufanya tathmini na kutoa msaada wa dharura unaohitajika katika maeneo hayo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa timu hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Mrakibu Agustine Magere amesema maeneo yaliyoathirika ni kata 10 za Manispaa ya Musoma ambazo ni; Kitaji, Iringo, Mwigobelo, Kamunyonge, Mukendo, Mwisenge, Kwangwa, Bweri, Rwamlimi na Nyakato.
Kamanda Magere amesema kutokana na athari ya tukio hilo, kikosi kiliamua kuifunga barabara ya Lumumba Manispaa ya Musoma baada ya nyaya na nguzo za umeme kuangukia katika barabara hiyo na kuzuia maeneo ya starehe yaliyoathirika katika tukio hilo kuendelea kutumika hadi hapo yatakapopewa idhini na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma baada ya kujiridhisha kuhusu usalama wake.
Bwana Magere amesema jumla ya watu wanne walijeruhiwa katika maafa hayo kutoka katika Kata ya Kitaji na watatu wakiwa ni wavulana wenye miaka 3-12 na mmoja mwanamke (43) na wote walipatiwa matibabu katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya.
Kamanda Magere amesema wananchi ambao makazi yao yameathirika wameshauriwa kuhama katika maeneo hayo na kutafuta makazi ya muda wakati wakiendelea kuyarejeshea majengo yao katika hali yake ya kawaida na kuwataka wananchi kupiga namba ya bure ya kikosi hicho 114 ili kupata msaada wa haraka kunapotokea ajali au majanga.
Vilevile, Kamanda Magere amesema tukio hilo limeathiri miundombinu mbalimbali ya Manispaa ya Musoma ikiwemo barabara, miundombinu ya maji na umeme na imeharibu majengo ya taasisi mbalimbali ikiwemo ofisi za TANESCO, ofisi ya TTCL Mkoa wa Mara, majengo ya biashara na kuhudumia abiria katika Uwanja wa Ndege Musoma.
Majengo mengine ni majengo ya shule tano za msingi ikiwemo bweni moja la wanafunzi wenye mahitaji maalum lililokuwa linajengwa na mfadhili Shirika la Support Build for Student with Disability, Ofisi ya Mtendaji Kata ya Kitaji, Kanisa Katoliki, Msikiti katika eneo la Iringo na Kituo cha Polisi Kitaji.
Kamanda Magere amesema katika tukio hilo pia baadhi ya maeneo ya biashara kama vile maduka, kumbi za starehe, kituo cha mafuta (TANOIL) kilichopo Barabara ya Uhuru nacho kiliathiriwa na tukio hilo.
Aidha, jumla ya kaya 319 kutoka Kata 10 za Manispaa ya Musoma zimeathiriwa na tukio hilo lililotokea tarehe 23 Machi, 2025 na jitihada mbalimbali za kurejesha hali ilivyokuwa na usalama wa wananchi katika eneo hilo zinaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa