Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara leo imeanza ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 katika Mkoa wa Mara na kuipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa ilani hiyo.
Akizungumza katika ziara ya kamati hiyo Wilaya ya Rorya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa amesema miradi ya maendeleo yote aliyoikagua imetekelezwa vizuri na value for money katika miradi hiyo inaonekana.
“Mimi nimeridhika na utekelezaji wa miradi hii na ninaipongeza Serikali na watekelezaji na wasimamizi wa miradi kwa namna walivyotekeleza miradi hii katika Wilaya ya Rorya na kama Chama tumeridhika” amesema Mhe. Chandi Marwa.
Mhe. Chandi Marwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, viongozi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya na watendaji wa Serikali kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo yenye tija ambayo inakisaidia Chama kuaminika kwa wananchi.
Mhe. Chandi Marwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara kufuatilia upelekaji wa huduma za umeme na maji katika miradi ya VETA na Shule ya Sekondari ya Jaffari Chege inayoendelea kujengwa ili kuwepo na huduma hizo wakati zitakapoanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi.
Katika mradi wamiundombinu ya kilimo cha umwagiliaji Labour, Mhe. Chandi ameitaka Serikali kumsimamia mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa haraka ili wananchi waweze kufaidika na mradi huo kwa kulima kilimo cha uhakika na kudhibiti ng’ombe wanaoingia katika maeneo hayo ili kulinda miundombinu iliyowekwa.
Akiwa katika mradi wa Maji Nyamunga, Mhe. Chandi pia amewasalimia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyamunga na kutoa shilingi 500,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya michezo baada ya wanafunzi kumwambia uwepo wa hitaji la vifaa vya michezo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Meja Edward Gowelle amekipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kutenga muda wa kukagua miradi inayotekelezwa na Serikali na kuwakaribisha viongozi wa CCM kukagua na kutoa maoni na maelekezo ya namna bora ya kutekeleza miradi hiyo.
“Sisi tunakipongeza sana Chama cha Mapinduzi kwa kupata muda wa kukagua miradi inayotekelezwa na Serikali yake na tupo tayari kupokea maoni na maelekezo kuhusiana na utekelezaji wa miradi hii” amesema Mhe. Gowelle.
Katika Wilaya ya Rorya Kamati ya Siasa ya Mkoa imekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA Rorya, mradi wa maji ya bomba Nyamunga, ujenzi wa Shule ya Sekondari Jaffari Chege na mradi wa kilimo cha umwagiliaji Labour na kesho inaendelea katika Wilaya ya Tarime.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ambao wamejigawa katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeongozwa na Mhe. Chandi Marwa, kundi la pili limeongozwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mara Mhe. Iddi Mkoa huku kundi la tatu limeongozwa na Mjumbe wa NEC Mhe. Christopher Gachuma na kufanya ukaguzi katika Wilaya za Rorya, Serengeti na Musoma.
Kesho tarehe 21 Mei, 2025 Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara itahitimisha ukaguzi wake kwa kutembelea miradi katika Wilaya za Tarime, Bunda na Butiama.
Kwa upande wa Rorya, ziara hiyo imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, baadhi ya Watendaji wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Mwenyekiti, Mkurugenzi Mtendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Rorya na wasimamizi wa miradi iliyotembelewa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa