Balozi Maimuna Kibenga Tarishi leo ameongoza kikao kati ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi na wadau wa kodi wa Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwembeni Complex, Manispaa ya Musoma na kuwataka wananchi na wadau wa kodi Mkoa wa Mara kushiriki kutoa maoni kwenye Tume hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Tarishi amewataka wananchi na wadau wa kodi wa Mkoa wa Mara kutoa maoni katika mifumo mbalimbali iliyowekwa na Tume hiyo ili kuweza kusaidia katika maboresho ya mfumo wa kodi unaofaa kutumika hapa nchini.
“Hii ni nafasi ya kipekee Mhe. Rais ametupatia Watanzania kuweza kutoa maoni, kero, changamoto na mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa kodi hapa nchini, tuitumie kikamilifu na tushiriki zoezi hili kwa manufaa ya nchi yetu” amesema Balozi Tarishi.
Balozi Tarishi amesema Tume hiyo imejipanga kuwafikia watu wengi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ili kupata maoni, kero, changamoto na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi kwa kuzungumza nao, kupokea maoni kwa njia ya ujumbe wa simu za mkononi, barua pepe, dodoso la mtandaoni na Tovuti ya tume hiyo.
Balozi Tarishi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda na kuizindua tume hiyo tarehe 4 Oktoba, 2024 ili kuandaa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha mfumo wa kodi hapa nchini baada ya Serikali kupokea kwa nyakati tofauti tofauti malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na kodi.
Aidha, Balozi Tarishi ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara kwa maandalizi mazuri ya kikao hicho na kuwashukuru washiriki kwa ushiriki mzuri wa kikao ikiwa ni pamoja na kutoa michango ya kuboresha mfumo wa kodi hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Khalfan Haule ameishukuru Tume hiyo kwa kuwatembelea wadau wa kodi na kusikiliza maoni na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi hapa nchini.
Mhe. Haule amewashukuru washiriki wa kikao hicho kwa kutoa maoni ambayo yanaenda kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi hapa nchini na kuwataka waendelee kushiriki kutoa maoni kupitia kwenye mitandao kama walivyoelekezwa na tume hiyo.
Kwa upande wake, Bibi Judith M. Lugembe, Mmiliki wa Kiwanda cha Sabuni cha Lubasa na mshiriki wa kikao hicho ameiomba Serikali kutafuta uwezekano wa kuwafanya wafanya biashara kufungua akaunti za biashara na kodi zao kukatwa katika akaunti hizo kulingana na mapato na matumizi ya kampuni hizo.
Bibi Lugembe amesema kwa hali ilivyo kwa sasa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamekuwa wakiwalipisha kodi kwa kukadilia jambo ambalo amesema wafanyabiashara wengi hawalipi mapato halisi Serikalini na badala yake wanatoa rushwa ili wapewe makadirio kidogo ya kodi.
Aidha, ameiomba Serikali kuangalia kampuni zinazotoa mashine za EFD ambazo amesema zinakuwa kero kwa wafanyabiashara kwani kila mwaka wafanyabiashara wanatakiwa kuzinunua upya kwa shilingi 145,000.
Bibi Lugembe ameishauri Serikali pia kuunda Kamati ya Ushauri ya Kodi ya Mkoa ambayo itashughulikia changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara katika Mkoa husika badala ya hali ilivyo hivi sasa ambapo kama kuna changamoto inabidi mfanyabiashara akate rufaa ya kikodi.
Wajumbe wengine wa tume hiyo walioshiriki kikao hicho ni Prof. Mussa Assaad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mstaafu na Prof. Florens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Mstaafu pamoja na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Tume hiyo.
Malengo ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ambayo Mwenyekiti wake ni Balozi Ombeni Yohana Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu ni pamoja na kuchambua Sera na Sheria za kodi na kubaini maeneo ya kuboresha, kubaini athari za viwango vya kodi katika sekta ya uchumi, kufanya mapitio ya mifumo na mbinu za ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi na kuchambua usimamizi na utekelezaji wa sheria za kodi na kuchambua mapato yasiyo ya kodi yanavyoathiri sekta za uzalishaji.
Malengo mengine ni kuainisha changamoto zinazoathiri utendaji wa mamlaka zinazosimamia ukusanyaji wa kodi, ushuru, tozo na ada mbalimbali, kuchambua usimamizi wa mapato ya mamlaka za udhibiti na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kupokea na kuchambua maoni ya wananchi na wadau, kupata uzoefu kutoka kwenye nchi nyingine kuhusu masuala ya kodi na kuandaa taarifa jumuishi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa