Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amezungumzia maendeleo ya uchunguzi uliokuwa unafanyika kuhusiana na watu waliohisiwa kukwama chini ya Mgodi wa North Mara walipoingia humo kwa nia ya kuiba.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 9 Aprili 2021 Mheshimiwa Malima amesema kuwa kwa sasa hamna watu waliokwama chini ya mgodi lakini uchunguzi unaonyesha kuwa kulikuwa na watu walioingia na kutoka chini ya mgodi huo.
“Kwa sasa vyombo vya dola vinahitaji kuwahoji watuhumiwa watano ambao walikuwa wanajihusisha na kufadhili makundi ya vijana waliokuwa wanakwenda kuiba ndani ya Mgodi wa North Mara kwa mahojiano zaidi” alisema Mheshimiwa Malima.
Amewataja watuhumiwa kuwa ni Bwana Rafael Matiku Zakaria ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la Bweri, Manispaa ya Musoma; Bwana Keraha Yohana Shona ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime na Bwana Manase Kazota Philemon mkazi wa Buswelu mkoani Mwanza.
Watuhumiwa wengine ni wanaohitajika katika ukamilishaji wa uchunguzi huo ni Bwana Makenge Chacha Nyaisa mkazi wa Nyamwaga, Tarime na Bwana Nyagwisi Charles Marwa Mkazi wa Tarime.
“Watuhumiwa wote hawa wanatakiwa kujisalimisha katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara au Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/Rorya haraka iwezekanavyo kabla jeshi halijaanza kuwatafuta” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa kwa pamoja wamekuwa wakifadhili baadhi ya vijana kuingia katika Mgodi wa North Mara unaomilikiwa kiubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya Barrick.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Malima ameongelea kuhusiana na maendeleo ya uchunguzi wa udanganyifu uliofanyika katika malipo ya fidia kwa wananchi wa vijiji viwili katika eneo la Nyamongo.
“Uchunguzi umefikia katika hatua nzuri na kwa sasa watuhumiwa 16 wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili” alisema Malima.
Ameeleza kuwa mpaka sasa uchunguzi umebaini katika ya fedha zote zaidi ya bilioni 30 zilizolipwa fidia, zaidi ya bilioni mbili zililipwa kwa watu waliotoa vielelezo visivyo sahihi na hivyo hawastahili malipo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa