Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema kuwa pamoja na Mkoa wake kufanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa kitaifa kidato cha sita mwaka huu lakini bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo ya kitaifa.
Akipokea vikombe vya ushindi kwa michezo ambayo timu za Mkoa wa Mara zilipata kwenye mashindano ya Umisseta na Umitashumita mwaka huu, Malima amesema kuwa Mkoa bado una nafasi ya kufanya vizuri endapo kila mmoja wetu atatimiza majukumu na wajibu wake kama inavyotakiwa. Ni lazima mikakati, ufuatiliaji na usimamizi wa nidhamu kwa walimu na wanafunzi vifanyike kwa ukaribu zaidi ili kuweza kupiga hatua kutoka hapa tulipo , alisema Malima.
Aidha ,Malima aliwataka walimu Mkoani Mara kujipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa Mkoa unafanya vizuri kitaaluma kwa manufaa ya watoto wa Mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla. “Haiwezekani tuwe tunafanya vizuri katika Michezo lakini kwenye taaluma tunashika mikia. Ni lazima Mkoa ujipange ili jitihada zilizotumika katika kuhakikisha Mkoa unafanya vizuri kwenye michezo ya Umisseta na Umitashumita iliyofanyika kitaifa Mkoani Mtwara na kupelekea Mkoa wa Mara kuwa mshindi wa tatu kitaifa zitumike pia katika kuhakikisha kuwa Mkoa unafanya vizuri kitaaluma na kupandisha ufaulu katika mitihani ya kitaifa kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.”alisisitiza Malima.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Afisa elimu wa Mkoa wa Mara Bw. Emmanuel Kisongo amesema licha ya kufanya vizuri katika Michezo ,Mkoa umeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha ufaulu unapanda kwenye mitihani ijayo ya kitaifa.
“Ni kweli kuwa hatujafanya vizuri kwenye taaluma kama Mkoa na hilo halina ubishi ,lakini tunajipanga na kuendelea kusisitizana kila mmoja wetu awajibike anapostahili ili tutokane na aibu hii.”alisema Kisongo.
Mkoa wa Mara ni Mkoa mkongwe ambapo muasisi wa taifa hili Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere alizaliwa.Ni moja ya Mikoa iliyoka kanda ya ziwa.
Imeandaliwa na
Stephano Amoni
Afisa Habari –Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa